Wednesday 3 March 2010

Mahojiano ya KLH News na Mheshimiwa Philip Marmo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge) Bw. Phillip Marmo (pichani) amesema kuwa serikali haitokaidi uamuzi wa Mahakama kuhusu suala la wagombea binafsi endapo Mahakama ya Rufani itasisitiza kuwa waruhusiwe kwenye uchaguzi mkuu ujao kama ilivyoamuriwa na Mahakama Kuu mwaka 2005.
Hata hivyo, Bw. Marmo amesema kuwa kutokana na mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mkuu kufikia mbali endapo msimamo wa mahakama utakuwa ni ule ule basi itabidi uchaguzi mkuu uahirishwe ili kuruhusu utaratibu wa kubadili Katiba na kuwezesha wagombe huru na binafsi kushiriki kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu.

Pamoja na hilo Bw. Marmo amedokeza kuwa endapo itabidi Katiba ibadilishwe basi kuna uwezekano kuwa suala la mgombea binafsi litarudishwa kwa wananchi ili liamuliwe kwa kupitia kura za maoni. Akizungumza na KLHN International ambacho ni kituo cha Watanzania kirushacho matango kupitia mtandao wa Intaneti Bw. Marmo alisema kuwa hata hivyo kwa wakati huu suala la kura za maoni halipo “kwani tutavuka huo mto tukiufikia”.

Kuhusu kile ambacho kinaonekana kuwa ni mgongano kati ya serikali na mahakama kuhusu suala la mgombea binafsi Bw. Marmo alisema kuwa hakuna mgongano wowote isipokuwa hivi sasa haupo muda wa kutekeleza uamuzi wa mahakama akidai kuwa rufaa iliyokatwa na serikali ilisababisha uamuzi wa awali usitekelezeke.
Bw. Marmo alitumia mfano wa adhabu ya kifo ambapo rufaa ikikatwa basi adhabu ya awali ya kunyongwa haitekelezwi hadi rufaa iamuliwe. Hata hivyo alipoulizwa kwa kutumia mfano wa kesi ya Nalaila Kiula (aliyekuwa Waziri wa Ujenzi) na ile ya kina Nguza Viking ambapo wote licha ya kukata rufaa bado waliendelea kutumia adhabu zao Bw. Marmo alidai kuwa “kesi hizo ni za mazingira tofauti”.