Thursday 20 March 2008

Tutapata maji kweli?

Baadhi ya wakazi wa Meatu mkoa wa Shinyanga wakisubiri kuchota maji. Kumekuwa na matatizo ya maji katika eneo hilo jambo linalofanya wananchi wa Wilaya hiyo kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Mwanamke naye yumo

Usafiri Moro Leo si mchezo!

Hapa sawa!

Nunueni hata kimoja basi!

Uwanja wa MUM

Sehemu ya kukaa watazamaji katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM).

Mjadala ni popote

Wednesday 19 March 2008

Hapa juu nasi 'twaona'

Baadhi wananchi wa Maswa mkoa wa Shinyanga waliojitokeza kumsikiliza aliyekuwa Waziri wa Maji Dk. Shukuru Kawambwa huku wengine wakiwa juu ya miti.

'Jamani Maalbino'

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Zelothe Steven akionesha mifupa ya Albino. Kwa muda sasa kumekuwa na mauaji ya Maalbino katika baadhi ya mikoa nchini Tanzania kutokana na imani za kichawi.

Mambo ya Udaku nayo!

Hili ni moja ya magazeti ya Udaku (Gazeti Pendwa) ambayo yamekuwa yakidaiwa kuandika habari binafsi za watu kama linavyoonekana.

Hapa ni kazi tu

Wafanyakazi wakiendelea na ujenzi wa Bwawa la New Solar lililopo wilaya ya Maswa mkoa wa Shinyanga ambalo liko katika hatua za mwisho za ujenzi. Niliinasa picha hii nilipokuwa katika ziara na Dk. Shukuru Kawambwa alipokuwa Waziri wa Maji.

Tuesday 18 March 2008

MUM nao 'wamo'


Gazeti hili la TAFAKURI hutolewa na baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM) Kitivo cha Mawasiliano ya Umma mwaka wa tatu . Hii ni siku moja baada ya uchaguzi wa kumtafuta Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi ya Chuo hicho (MUMSO). Utolewaji wa gazeti hili ni ishara dhahiri kuwa chuo hicho cha Waislamu 'kimewapika' vijana wake kuingia katika soko la ajira. Mhariri Mtendaji wa gazeti hili ni Abdulwakil Saiboko, Msanifu Kurasa Haji Athuman na Mhariri Mshiriki ni mimi.

Hali hii mpaka lini?

Wafanyabiashara wa ndizi katika kituo cha mabasi cha Msamvu wakijikinga kwa Miamvuli wakati wakisubiri wateja.

Msamvu

Hapa ni mzunguko wa magari katika eneo la Msamvu Morogoro ambapo mabasi ya abiria yanayoenda na kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati hupita hapo

Mwanamke kikapu!

Hivi ni vikapu vinavyouzwa katika kituo cha mabasi cha Msamvu mkoani Morogoro.Wanawake wamekuwa wakisisitizwa kutumia vikapu waendapo kununua bidhaa maeneo mbalimbali.

Unyanyapaa


Vijana kama hawa huwezi kuwasahau wakati wa jitihada za kupiga vita unyanyapaa dhidi ya wagonjwa wenye ukimwi.

Mnaniona?

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Arusha Meru akionesha umahiri wa kucheza mbele ya wageni waalikwa wakati wa Mahafali ya kidato cha sita shuleni hapo. Picha hii ni kwa hisani ya Jamal Hashim.

Na sisi tunayaweza

Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Arusha Meru ya mkoani Arusha wakionesha umaarufu wa kusakata muziki wa Kimarekani. Hapa ilikuwa ni katika mahafali ya kidato cha sita shuleni hapo. Picha hii ni kwa hisani ya Jamal Hashim.

Monday 17 March 2008

Kilwa

Dk. Shukuru Kawambwa anayeangalia mbele akimsikiliza mkuu wa wilaya ya Kilwa Bw. Nurdin Babu. Hapa ilikuwa ofisini kwa mkuu wa wilaya mkoa wa Lindi wakati Dk. Kawambwa alipotembelea wilaya hiyo alipokuwa Waziri wa Maji.

Sote tunawajibika

Mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Bi. Ester akijitolea kutoa damu kwa ajili ya Benki ya damu Muhimbili.

Mambo ni hivi!


Rais wa Jumuiya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Waislamu Morogoro(MUMSO) Bw. Khamis Rajabu akionesha msisitizo mara baada ya kutangazwa kuwa kiongozi wa jumuiya hiyo. Bw. Rajabu ameshika nafasi hiyo baada ya Rais Siraji Jafari kumaliza kipindi chake cha uongozi. picha hii ni kwa hisani ya Abdulwakil Saiboko.

'Rais'

Rais mpya wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Cha Waislamu Morogoro (MUMSO) Khamis Rajabu (kushoto) na Makamu wake Shekha Khamis muda mfupi baada ya kutangazwa kushika nyadhifa hizo jana. Picha hii ni kwa hisani ya Abdulwakil Saiboko.

Furaha

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro wakifurahia ushindi alioupata Hamis Rajabu katika kinyang'anyiro cha urais wa MUMSO. Bw. Rajabu alimshinda Mzee Mzee na hivyo kuukwaa wadhifa huo. Hii picha ni kwa hisani ya Abdulwakil Saiboko.

Sunday 16 March 2008

Ajali

Hii ni gari ambayo mtoto wa Bakharessa alipoteza maisha wakati wa mashindano ya magari mjini Zanzibar.

Ukosefu wa maji huleta umasikini

Unapozungumzia umasikini basi ieleweke kuwa ni jambo linalozikabili nchini nyingi hususan zile nchi za dunia ya tatu Tanzania ikiwemo. Yapo mambo mengi yanayozungumzwa kuwa yanachangia kwa namna moja ama nyingine kushamiri kwa umasikini lakini kwa mtazamo wa wazi ukosefu wa maji unaweza kuwa moja ya sababu kubwa zinazochangia umasikini duniani.

Ieleweke kuwa Ulimwengu wote sasa unakabiliwa na upungufu wa maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu ikiwa ni pamoja na matumizi ya nyumbani, kilimo, usindikaji bidhaa viwandani na uzalishaji umeme. Kwa ujumla upungufu huo wa maji unaathiri maisha ya binadamu na mazingira.

Mbali na maji kuwa muhimu bado tunayapunguza kwa kuyamwaga ovyo, kuchafua vyanzo vyake, kukata misitu, kuchimba miamba hasa kwenye shughuli za uchimbaji madini pamoja na kutumia teknolojia za uzalishaji zinazotumia maji kidogo hasa viwandani na kwenye kilimo.

Maji ndiyo mhimili mkuu wa uchumi na yanapopungua husababisha umasikini wa kukithiri hivyo ni wajibu yatunzwe na kutumika kwa umakini.

Kwa kawaida mahitaji maji yanaongezeka wakati maji yenyewe yanapungua hali hiyo inasababisha migogoro katika jamii na migogoro hiyo inaweza kuwa kati ya watumiaji mbalimbali wa maji na nchi zinazomiliki vyanzo vya maji kwa pamoja hivyo jamii yoyote ikishakuwa na mgogoro haiwezi kufanya kazi yoyote ya uzalishaji na kuishia kuhangaikia umasikini.

Kwa kuwa maji ni muhimu, jamii nyingi zisizokuwa na huduma ya maji hutumia muda mrefu kutayatafuta badala ya kushughulikia masuala ya maendeleo, kwa maana nyingine mapungufu ya maji kwenye mito na mabonde hupunguza uzalishaji wa chakula hasa kwa wale wenye mashamba yanayozalisha kwa mwagiliaji.

Kwa zile sehemu zenye uhaba, maji huchotwa bila kubakizwa kwa ajili ya utunzaji mazingira hali inayosababisha wanyama na viumbe wengine kufa au kuhama.Kuna maeneo mengine vyanzo vya maji hutumika kupokea uchafu toka majumbani au kwenye mabwaya ya kusafishia maji taka.

Jamii ikikumbwa na janga la upungufu wa maji mara nyingi hutangatanga kama ilivyojitokeza nchini Tanzania mwaka 2006 ambapo wafugaji waliacha makazi yao na mali nyingine wakahama kutafuta maji. Jamii hii ilipoteza mifugo na kukosa huduma muhimu kama shule, hospitali na maduka ya kupata mahitaji.

Hali ya maji Tanzania inaonesha kuwa hadi kufikia Desemnba 2006 huduma ya upatikanaji maji mijini ilikuwa asilimia 78 na vijijini ni 55 wakati maji taka mijini ni asilimia 17 ingawa kiwango nkilichoainishwa ni kidogo lakini bado nchi ina vyanzo vya maji vya kutosha.

Hata hivyo, utafiti unaonesha kuwa tukigawana maji yanayoingia kwenye vyanzo vya maji kwa mwaka kila mtanzania atapata lita milioni 2.7 kwa mwaka ambayo ni sawa na lita 670 kwa siku inayojumuisha matumizi ya maji yote. Ingwa Tanzania kuna maji mengi lakini hayajasambaa kwa usawa katika sehemu zote nchini kwani Sehemu za kati kati ya nchi zinapata mvua kidogo ukilinganisha na maeneo mengine..

Katika mfumo wa usambazaji maji nchini kwa matumizi ya kawaida inakadiriwa kupoteza wastani wa asilimia 30-50 huku umwagiliaji nao ukichukua asilimia 70-85. Sehemu nyingine zinajumuisha uharibifu miundo mbinu, ukosefu wa kufanya matengenezo wa mfumo wa usambazaji pamoja na kutolipwa kwa gharama halisi ya kupata maji.

Hata hivyo, mbinu mbalimbali zinaweza kutumika ili kupunguza upotevu wa maji na baadhi yake ni kutumia maji kidogo, kupanga mipango ya matumizi ya ardhi inayozingatia uhifadhi wa vyanzo vya maji , kutumia maji kwa uangalifu, kupunguza yanayovuja, kuchagua teknolojia isiyotumia maji mengi , kuchagua kilimo kisichotumia maji mengi na kuwa na mifugo inayolingana na uwezo wa eneo.

Aidha, vyanzo vya maji mbadala pia ni muhimu katika kupambana na upungufu wa maji vyanzo hivyo ni pamoja kusafisha maji taka, kutumia maji ya bahari, kuchimba visima virefu hadi vya mita 1000 kwenda chini ya ardhi, kutumia wataalamu wa kumwagia mashamba wa matope(drip irrigation)

Vile vile, kuhusisha jamii katika kubuni, kujenga na kuendesha miradi ya maji hasa maeneo ya vijijini. Utaratibu huu utaimarisha uwezo wa wananchi kumiliki na hivyo kupunguza uchimbaji wa miundo mbinu .

Elimu kwa watu wa mijini itiliwe mkazo huku watu hao wakielimishwa umuhimu wa kulipa Ankara za maji wanayotumia, utunzaji ushirikishe sekta nyingine zinazohusika na matumizi ya vyanzo hivyo mfano sekta ya kilimo na ufugaji, misitu, madini na ardhi.

Kwa kuhitimisaha naweza kusema kuwa upatikanaji maji ya kutosha na salama kwa matumizi mbalimbali ni muhimu katika kuleta maendeleo ya kupunguza umasikini hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kupambana na tatizo la upungufu wa maji katika kuleta maendeleo, kuondoa umasikini , kupunguza maradhi sambamba na kuongeza uzalishaji mashambani na viwandani.

Matumizi sahihi ya maji ni kupunguza upotevu wa maji utakaowezesha taasisi zinazosimamia na kutoa huduma ya maji kupata fedha za kufanya matengenezo na kupanua miundombinu.

Mji kasoro Bahari

Sehemu ya mji wa Morogoro

Akina mama

Akina mama nao hawako nyuma katika shughuli za maendeleo kama wanavyoonekana hawa wa kijiji cha Nyakabindi Wilayani Bariadi mkoa wa Shinyanga walipojitokeza wakati wa uzinduzi wa visima vya maji.

Bwawa


Bwawa la Mwanyahina lilipo Wilayani Meatu mkoa wa Shinyanga. Maji ya bwawa hili yanatumiwa na wakazi wa Meatu.

Soka

Wachezaji wa timu ya soka ya Kitivo cha Elimu mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro wakipasha misuli moto kabla ya mpambano wao na wenzao wa mwaka wa kwanza.

Watoto

Watoto wanaoishi Wilaya ya Meatu mkoa wa Shinyanga wakichota maji yanayotoka bwawa la Mwanyahina.

Ngoma

Kikundi cha ngoma cha Mgambo kilichopo wilayani Maswa mkoa wa Shinyanga kikiwatumbuiza wananchi wa wilaya hiyo wakati wa Ziara ya Waziri wa Maji.

'Hapo vipi'

Dk. Shukuru Kawambwa 'akipampu' maji ya kisima Wilayani Bariadi mkoa wa Shinyanga. Wa kwanza kushoto ni mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dk. Brigedia Jenerali Yohana Balele na katikati ni mkuu wa wilaya ya Bariadi Baraka Konisaga.

Tuwaenzi wazee

Bw. Rashid Singano wa Kijiji cha Dule wilaya ya Lushoto mkoa wa Tanga.

Mbunge huyu awe mfano

Dk. Shukuru Kawambwa akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa Same Mashariki wakati akizindua miradi ya maji ya kisima iliyojengwa kwa juhudi za mbunge wa jimbo hilo Bi. Anne Kilango Malecela.



Mwishoni mwa mwaka 2007 aliyekuwa Waziri wa Maji Dk. Shukuru Kawambwa alifanya ziara katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Mara na Shinyanga, ziara iliyokuwa na lengo la kukagua ujenzi wa miradi ya maji pamoja na kuzindua visima vya maji.

Kati ya mikoa hiyo aliyotembelea mhe. Waziri wa Maji mkoa wa Kilimanjaro ziara yake ilielemea zaidi kwenye uzinduzi wa visima tofauti na mikoa mingine.

Wilayani Same katika jimbo la Same Mashariki Dk. Kawambwa alizindua jumla ya visima ishirini vyenye thamani ya shilingi milioni 40 kwenye tarafa ya Gonja katika zile kata za Mtii, Bombo, Vuje pamoja na ile tarafa ya Ndugu kata ya Kihurio.

Visima vyote alivyozindua Dk. Kawambwa vimefungwa kwa pampu za mkono na kufuata vyanzo vya asili lengo likiwa kurahisisha upatikanaji maji hasa ikizingatiwa upatiakanaji maji chini ya ardhi ya milima ni migumu.

Miradi hiyo ya visima iliyozinduliwa Wilayani Same imeinua asilimia ya upatikanaji wa maji ya bomba kutoka makisio ya asilimia 5 katika kata ya Mtii hadi 30, asilimia 20 kata ya Vuje hadi 35, asilimia 43 kata ya Kihurio hadi 62 na ile asilimia 12 kata ya Bombo hadi 25.

Kwa sasa asilimia 70 ya wananchi wa jimbo la Same Mashariki wanaishi milimani ambako kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa maji na kusababaisha asilimia 30 ya wakazi wa eneo hilo kupata magojwa yanayotokana na maji yasiyo salama.

Kwa ujumla wilayani Same kuna matatizo ya maji ambapo eneo la Tambararre ya Pare na milima ya kijiji cha Kizungo linakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.

Wakati wa ziara yake katika jimbo hilo la Same Mashariki Dk. Kawambwa alipongeza jitihada binafsi za mbunge wa jimbo la Same Mashariki Bi. Anne Kilango Malecela za kuasaidia upatikanaji huduma za majisafi na salama katika jimbo lake kutoka asilimia 46.5% hadi 49%

Pongezi hizo za Waziri wa Maji kwa mhe. Anne Kilango Malecela zinastahili kabisa kwa kuwa mbunge huyo alipagana kufa na kupona kuhakikisha anawapatia wapiga kura wake huduma ya majisafi pasipo kuitegemea zaidi serikali.

Nilipozungumza naye, mbunge huyo wa jimbo la Same Mashariki alisema anajisikia faraja sana anapoona wapiga kura wake wanapata huduma ya majisafi na salama jambo alilosema lilikuwa likimuumiza kichwa kwa muda mrefu.

Aliongeza kwa kusema, upatikanaji huduma hiyo ni jitihada yake binafsi ya kusaka wafadhili wa kumsaidia kuwapatia huduma hiyo ya maji wananchi wake ambayo imekuwa adimu jimboni mwake na wilaya nzima ya Same.

Aliyataja baadhi ya makampuni yaliyomsaidia kufadhili ujenzi wa miradi hiyo ya visima kuwa ni kampuni za simu za Tigo na Vidacom, mamlaka ya Bandari Tanzania (PTA) pamoja na kampuni ya kifaransa ya Express Lited.

‘’Makampuni ya ndani nayo yanafadhili sana ili mradi mtu ujue namna ya kuandika proposal yako’’ Alisema Bi. Kilango

Alieleza kuwa, mkakati wake wa kuawapatia wananchi wa jimbo la Same Mashariki huduma ya majisafi umelenga kwenda kata hadi kata na kuongeza kuwa yeye akiwa mbunge atajisikia faraja sana pale atakapoona wapiga kura wake wanapata huduma ya majisafi na salama katika kiwango cha asilimia mia moja.

Kwa upande wake Dk. Kawambwa alisema katika kuhakikisha tatizo la maji linatokomezwa mkoani Kilimanjaro serikali iko mbioni kuanzisha mradi mkubwa wa kitaifa unaojulikana kama mradi wa Tambararre ya Pare, mradi unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 38.

Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, mradi huo utakapokamilika utanufaisha vijiji 36 kutoka wilaya za Same na Mwanga zilizoko mkoani Kilimanjaro na ile sehemu ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Vijiji vitakavyonufaika na mradi huo mkubwa ni vile vya Hedaru, Mabilioni, Gevao, Makanya,Mgurasi,Bangalala,Chajo,Mwembe,Njoro,Ruvu mferejini,Ruvu jiungeni,Majengo,Bendera,Mkonga Ijinyu na Mgandu vyote kutoka wilaya ya Same.

Vingine ni Kifaru,Kiruru Ibwejewa,Kisangara, Lembeni , Kiverenge,Kiti cha Mungu,Mbambua, Kileo,Kivulini,Kituri,Mgagao,Handeni,Langata Bora,Langata Kangongo, Nyabinda na kijiji cha Kirya vyote kutoka Wilaya ya Mwanga.

Kwa upande wa Wilaya ya Korogwe maeneo yatakayofaidika ni vijiji vya Bwiko,Mkomazi, Nanyogie,Manga, Mtindilio na Mikocheni

Waziri huyo wa Maji alibainisha kuwa, katika kuhakikisha mradi huo unaanza haraka tayari serikali imeomba ufadhili wa mradi huo kutoka Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA) ili isaidia ujenzi wa mradi.

Mbali na jitihada zinazooneshwa na serikali kuwapatia wananchi wa Wilaya ya Same huduma ya majisafi na salama lakini bado juhudi binafsi zilizooneshwa na mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Bi. Anne Kilango Malecela ambaye hivi karibuni alijipatia umaarufu katika sakata la Richmond zinapaswa kuigwa na wabunge wengine wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mara kwa mara tunashuhudia malalamiko ya baadhi ya wabunge kuilaumu serikali kushindwa kupeleka huduma kwa wananchi ikiwemo huduma ya majisafi na salama, kwa kiasi fulani lawama hizo zinaweza kustahili lakini isiwe kigezo cha mbunge kuacha kufanya juhudi za kuwapelekea maendeleo wapiga kura wake kwa kisingizio cha serikali kufanya kazi hiyo.

Iwapo wabunge wataiga mfano wa Bi. Anne Kilango Malecela basi uwezekano mkubwa wa Tanzania kupiga hatua katika nyanja tofauti ni mkubwa sana kwani kila mtu atakuwa anajua wajibu wake kama mbunge na kamwe hawezi kuwa tegemezi wa serikali.

Mbunge huyo machachari alisema mtazamo wake mkubwa kwa sasa kama mbunge ni kutaka kuwaona wapiga kura wake wakiishi maisha mazuri na kuondokana na umasikini na magonjwa ambavyo vyote kwa pamoja vinaweza kuwafanya warudi nyuma kimaisha.

Maji yaja Shinyanga

Bwawa la maji la Zanzui Wilayani Maswa mkoa wa Shinyanga ambalo liko katika hatua za mwisho kukamilika.

Mwishoni mwa mwaka jana (2007) aliyekuwa Waziri wa maji Dk. Shukuru Kawambwa alifanya ziara katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Mara na Shinyanga, lengo la ziara hiyo ilikuwa kukagua ujenzi wa miradi ya maji pamoja na kuzindua visima.

Katika ziara hiyo Waziri wa Maji alitembelea Wilaya za Same (Kilimanjaro), Bunda na Serengeti (Mara) pamoja na Bariadi, Maswa , Meatu na Kishapu (Shinyanga).

Dk. Kawambwa katika ziara yake hiyo alikagua mabwawa ya Nyambele na Kinyambwiga yaliyoko wilayani Bunda, Mugumu (Serengeti), Zanzui (Maswa) na bwawa la Mwanyahima lililopo Meatu.

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la uharakishaji upatikanaji maji safi na salama kuwa wananchi wa wilaya husika katika muda muafaka kama ilivyoainishwa katika Sera ya Maji ya mwaka 2006-2025.

Miradi yote aliyoikagua Dk. Kawambwa pamoja na ule mradi mkubwa wa maji wa Kahama-Shinyanga inatarajiwa kukamilika mwaka huu 2008 na mara itakapokamilika tatizo la maji katika mkoa wa Shinyanga linaweza kubaki historia.


Mbali na juhudi za kuupatia mkoa wa Shinyanga maji, Dk. Kawambwa alisema serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 359 kwa ajili ya kuboresha huduma ya majisafi na salama nchini Tanzania.

Alisema kupitia kiasi hicho cha pesa kila wilaya imetengewa fedha kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji na kueleza kuwa tayari shilingi bilioni 19.5 zimegawanywa mwaka 2007 kwa zile halmashauri zilizokidhi vigezo vya kupatiwa fedha hizo.


Hata hivyo, Dk. Kawambwa alisema bado wananchi wana deni kubwa kwa wafadhili na wahisani juu ya miradi ya maji inayozinduliwa na kueleza kuwa kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanaunda vyombo vya kisheria vitakavyosimamia na kuendesha miradi ya maji.

Cha msingi kwa wananchi wa Tanzania mara baada ya kukamilika kwa miradi yote ya maji ni kutunzwa sambamba na kuanzishwa kamati za maji zitakazokuwa na jukumu la kusimamia na kuiendesha miradi hiyo ili iwe endelevu.

Pia wananchi hawana budi kushirikiana na serikali kwa kuacha kuendesha shughuli zozote kwenye vyanzo vya maji ikiwemo ufugaji na shughuli nyingine ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaweza kusababisha vyanzo hivyo kuharibika.


Watoto

Khairat mbele na wenzake Yusufu na Kauthar wakionesha alama ya vyema wakiwa Dar es Salaam, Tanzania.

'Tunajichana'

Mtoto Kauthar akipata mlo na watu wengine kusheherekea siku yake ya kuzaliwa. Hapa ni London.

Ziara ya Dk. Kawambwa Misri iwe changamoto

Dk. Shukuru Kawambwa na Waziri wa Rasilimali za Maji na Umwagiliaji wa Misri Dk. Mahmoud Abu-Zeid wakisaini mkataba. Hapa ilikuwa jijini Cairo, Misri.


Hivi karibuni aliyekuwa Waziri wa Maji Dk. Shukuru Kawambwa alifanya ziara ya siku tano nchini Misri kwa mwaliko wa Waziri wa Rasilimali za Maji na Umwagiliaji wa Serikali ya Misri, Dkt Mahmoud Abu-Zeid.

Ziara hiyo ililenga kufuatilia utekelezaji wa maafikiano yaliyofikiwa baina ya Tanzania na Misri wakati wa ziara ya aliyekuwa waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo mwaka 2004, Mhe. Edward Lowassa, pamoja na kuangalia jinsi ya kuimarisha na kupanua ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Katika ziara hiyo Dk. Kawambwa na mwenyeji wake Dk. Abu-Zeid walipitia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa mwaka 2004, ambapo baadhi ya mambo yaliyokwishatekelezwa ni kupatiwa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalamu 16 wa kitanzania kuhusiana na maji shirikishi, mazingira, maji kwenye maeneo kame na kilimo cha umwagiliaji sambamba na mradi mpya wa kutathmini rasilimali za maji chini ya ardhi kwa Bonde la mto Nile kuanza kutekelezwa mwaka huu wa fedha 2007/2008.

Akiwa nchini Misri, Dk. Kawambwa na Dkt Abu-Zeid walisaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa uchimbaji visima 30 kwenye Wilaya kame nchini. Jumla ya Wilaya 6 zitanufaika na mradi huo. Wilaya hizo ni Same (Kilimanjaro), Kiteto(Manyara), Tarime na Bunda (Mara), Maswa (Shinyanga) na Magu (Mwanza).

Wakati wa utiaji saini mkataba huo, Mhe. Kawambwa aliwasilisha rasmi ombi kwa Serikali ya Misri kusaidia kuchimba visima vingine 70 kwenye maeneo kame nchini Tanzania ili kuwaondolea kero ya maji wananchi wa maeneo husika.

Uchimbaji huo visima siyo tu utawaondolea kero ya muda mrefu ya maji katika maeneo hayo bali utapunguza lawama za muda mrefu zinazoelekezwa kwa mamlaka husika pamoja na serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi kuwa imeshindwa kuwapatia majisafi na salama kama ilivyoainishwa katika ilani yake ya chama.

Mbali na kutiwa saini mkataba huo utakaoleta nafuu ya maji kwa wale wananchi wanaoishi maeneo kame tumaini lingine ni ile ahadi iliyotolewa na wataalamu washauri wa mradi wa maji Chalinze kuwa wanaandaa ratiba mpya itakayoonesha jinsi watakavyokamilisha kazi ya usanifu ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Ahadi hiyo inatokana na Dk. Kwambwa kutoa agizo kwa wataalamu washauri wa mradi huo wa Chalinze ambao ni Dk.Ahmed Abdel Warith Consulting Enginerrs, kampuni inayosanifu ujenzi wa mradi huo.

Wataalamu washauri hao bado walikuwa hawajawasilisha Wizarani taarifa muhimu za hatua ya kwanza, jambo lililoelezwa limekwamisha awamu ya pili ya mradi wa Chalinze kuanza katika muda uliopangwa suala lililomlazimu Dk. Kwambwa kuwataka washauri hao kuhakikisha usanifu unakamilika Novemba 30 mwaka huu ili kuruhusu zabuni za ujenzi kutabngazwa Desemba mwaka huu..

Pia Dk. Kawambwa na ujumbe wake walitembelea Kituo cha Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji, kituo kinachofuatilia hali ya hewa na rasilimali za maji nchini Misri ambapo madhumuni yake ni kupata takwimu muhimu kwa kutumia njia za kisasa kama Satelite kwa ajili ya kuzitumia katika usimamizi na udhibiti wa rasilimali za maji. Kituo hicho pia kinafuatilia miradi yote ya umwagiliaji ili kuwa na uwiano mzuri wa matumizi ya maji yanayopatikana.

Kituo hicho ni moja ya changamoto kwa Tanzania kuanza kufikiria namna ya kuwa na kituo cha aina hiyo ili kuweza kufuatilia hali ya hewa na rasilimali za maji kwa lengo la kufahamu na kuzitumia vyema rasilimali zilizopo hapa nchini kwa ajili ya kizazi kilichopo na kijacho.

Aidha, alitembelea pia Benki ya Taifa ya Takwimu za Rasilimali za Maji na Umwagiliaji, Benki hiyo ina taarifa zote kuhusu mitaro na njia zote za umwagiliaji wa maji kwenye mashamba, maji chini ya ardhi, uondoaji majitaka, majitaka kutoka viwandani, mazingira na hali ya uchumi.

Mbali na mambo mengine, Mhe. Kawambwa alipata nafasi ya kujionea kituo cha kutabiri masuala ya hali ya hewa na muelekeo kuhusu vyanzo vya maji ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana kutoka kwenye satellite, kituo hicho hutumika kutabiri muelekeo kuhusu mawingu na hatimaye makadirio ya kiasi cha mvua na maji kwenye kijibonde cha mto Nile. Takwimu hizo husaidia kukadiria kiasi cha maji yanayoingia kwenye bwawa la Aswani. Dk. Kawambwa na ujumbe wake walifarijika kuona umuhimu wa kuwepo kituo kama hicho nchini Tanzania kwa kuwa ni kiungo muhimu kwa ajili ya vyanzo vya maji.

Vile vile, Dk. Kawambwa na ujumbe wake walitembelea Kituo cha Kitaifa cha Tafiti za Maji chenye taasisi 12 chini ya udhamini wake. Baadhi ya Taasisi hizo ni Taasisi ya Tafiti za Rasilimali za Maji, Maabara Kuu ya Usimamizi wa Mazingira na Taasisi ya Tafiti kuhusu Miundombinu ya Maji iliyokubali kutoa msaada kwa Tanzania kufanya matengenezo ya vifaa vinavyotumika kupima wingi wa maji kwenye mito.

Alijionea pia mradi wa kuendeleza Sinai, mradi unaosimamiwa na Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji unaolenga kuanzisha maeneo mapya ya kilimo katika ekari 400,000 katika maeneo ya jangwa yaliyopo Sinai, lengo likiwa kupanua wigo wa Bonde la mto Nile na hivyo kuvutia wananchi kuhama kutoka Nile kwenda maeneo ya Sinai.

Ziara ya Waziri wa Maji ilihitimishwa kwa kutembelea shughuli za Kituo cha Kanda cha Mafunzo kwa Watumishi wa Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji nchini Misri, kituo kilichoanzishwa mnamo mwaka 1994 na kuchaguliwa na UNESCO 2002 kuwa Kituo cha Kanda kwa maeneo ya jangwa ya Afrika na nchi za Kiarabu na tayari kituo hicho kimekwisha kutoa mafunzo kwa wanafunzi kutoka Tanzani.

Yote haya aliyojionea Mhe. Kawambawa na ujumbe wake nchini Misri ni changamoto tosha kwa nchi yetu kuanza kuwa na mawazo ya kuwa na vitu vinavyoendana na teknolojia ya sasa katika kuafutialia na kuhifadhi rasilimali za maji ili kuepuka matatizo ya mara kwa mara ya ukosefu wa maji.

Hali hiyo inatokana na kuwa pamoja na Tanzania kuwa na matatizo ya maji lakini kuna taarifa kuwa Tanzania ni moja ya nchi katika Bara la Afrika yenye maji mengi chini ya ardhi ingawa bado hajagunduliwa.