Mbunge wa Igunga Mhe. Rostam Aziz (CCM) ameamua kulishtaki gazeti la Mwanahalisi na wakati huo huo kulitishia gazeti la Raia Mwema kuwa atalifungulia mashtaka endapo halitaomba radhi kwa mojawapo ya makala zake.
Bw. Rostam anakuwa kiongozi wa kwanza ambaye amekuwa akitajwa na vyombo vya habari kuhusu ufisadi aliyeamua kwenda mahakamani. Kwa namna ya pekee hli linaashiria mambo kadhaa.
Kwanza, endapo mahakama itaridhia maombi yake basi masuala ya Richmond na Rostam yanaweza yasitajwe kwenye sentensi moja kwani kesi itakuwa mahakamani . Huu ni mchakato wa Kisheria na vyombo husika vitatakiwa kuheshimu, ingawa hilo halitufungi sisi wengine kutolea maoni.
Pili, kujaribu kunyamazisha vyombo hivyo vya habari endapo kutakubaliwa na mahakama basi kutazuia habari mpya kuweza kuchapwa na gazeti hilo . Hata hivyo, sisi wengine tutaweza kuendelea kutolea maoni.
Jambo la tatu ni kuwa Bw. Rostam amefanya jambo la maana kwa kuamua kwenda mahakamani hasa kwa vile anaamini haki yake inatishiwa na jina lake kuchafuliwa. Hivyo, uamuzi wake ni mfano wa kuigwa kwa wengine ambao wanahisi kuonewa au kutotendewa haki ili watumie vyombo vya sheria kutafuta haki hiyo badala ya kukimbilia kwenye TV au radio kujisafisha.
Hata hivyo, kama kesi hii itanedelea au itaishia pembeni hatuna uhakika. Hata hivyo vyanzo vyangu vya karibu na MwanaHalisi vimenihakikishia kuwa hawana mpango wa ku "back down" na wanaendelea kufanyia kazi taarifa nyngine kuhusu Rostam na Richmond. Sisi wengine yetu ni macho tu.
Je wadaiwa wengine na wale wanaotajwa kwenye tuhuma za ufisadi na wenyewe waende mahakamani? Je ndiyo njia pekee ya wao kujisafisha? Kwanini wale wengine waliotishia kwenda mahakamani hawakwenda?