Saturday 29 March 2008

Mambo ya Lusaka

Hapa nikiwa na waandishi wenzangu katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Lusaka nchini Zambia, wa kwanza kulia ni John Wanyancha na katikati ni Omar Mtangilwa. Hii ilikuwa ni mwaka 2000.

Hii kali!


Bado tunakukumbuka


Hapa nipo na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu Dk. Omar Ali Juma. Hii ilikuwa mwaka 1999 nyumbani kwa Dk. Omar Oyesterbay Dar es Salaam.

Nimewakubali!

Mkuu wa Chuo cha Waislamu Morogoro (MUM) Bi. Mwantum Malale akizungumza na mtaalamu wa masuala ya ukaguzi kutoka nchini Uingereza Dk. Sarah Carthew. Mtaalamu huyo amekitembelea chuo hicho kwa ajili ya kukikagua kwa maendeleo ya baadaye.

Mambo ya Bush Africa

















Wednesday 26 March 2008

Upigaji ngoma huu!

Mpiga ngoma wa kikundi cha Sogea akipiga ngoma kwa 'staili' ya aina yake akiwa amekalia mti. Picha hii niliinasa Wilayani Masasi mkoa wa Mtwara.

Tuesday 25 March 2008

Tunamshukuru Mungu


Hapa rafiki yangu Thomas Mabeba (kulia) akiwa na Alfonce Mwakasege muda mfupi baada ya kutunukiwa shahada ya Utawala katika Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro. hii ilikuwa katika mahafali ya mwaka jana.

Tupo pamoja

Hapa nikiwa na Afisa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania Jaffery Salaiz (katikati) pamoja na Mkuu wa Kitivo cha Mawasiliano ya Umma Chuo Kikuu cha Wiaslamu Morogoro (MUM) Dk. Rajab (kushoto).

Mto huu utazamwe

Dk. Shukuru Kawambwa akiangalia jengo lililoharibiwa na mafuriko katika eneo la mto Mbwinji mkoani Mtwara. Jengo hilo lilikuwa likutumika kuhifadhia pampu ya kusukuma maji.

Dk. Shukuru Kawambwa akiangalia maji ya mto Mbwinji. Hapa ni wakati alipokuwa Waziri wa Maji.


Mbwinji! Mbwinji! Mbwinji! hayo ni maneno aliyokutana nayo aliyekuwa Waziri wa Maji Dk. Shukuru Kawambwa wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji katika mikoa ya Mtwara na Lindi hususan zile Wilaya za Masasi na Nachingwea.

Maneno hayo hayakuwa wimbo kwa Dk. Kawambwa bali yalikuwa ni imani kwa wakazi wa Masasi na Nachingwea juu ya chanzo cha maji cha mto Mbwinji kuwa kinaweza kuwaondolea kero ya maji inayowakabili wakazi wa maeneo hayo.

Mto Mbwinji ni muungano wa mito midogo midogo mitatu ambayo ni Mbwinji wenyewe, Rungwe na Minjale. Mito hii inatokana na chem chem za maji kutoka katika miteremko ya milima ya Makonde iliyopo Wilaya za Masasi na Newala kiasi cha kilometa kumi na mbili kutoka Ndanda kupitia barabara ya Miyuyu.

Kwa mujibu wa Afisa Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini Aloyce Kaponda, upimaji wa wingi wa maji katika mto huo hufanyika mara kwa mara kutokana na kukosekana kwa kituo cha kudumu cha kupimia maji, ukosefu wa fedha pamoja na ubovu wa barabara.

Kaponda alisema, kituo cha kudumu cha kupima maji kilisombwa na mafuriko ya mwaka 1990 hivyo jitihada za kujenga kituo kipya bado zinaendelea ambapo mwaka 2005 upimaji wa maji katika mto huo ulifanywa na chuo kikuu cha Dar es Slaam kama wataalamu wasahauri (Consultant) wa Halamashauri ya Wilaya ya Masasi lakini taarifa ya uchunguzi huo haikutolewa katika ofisi yake.

Upimaji wingi wa maji katika mto Mbwinji kwa mara ya mwisho ulifanyika Novemba 27, 2007 ikiwa ni mwisho kabisa wa kipindi cha kingazi na kuchukuliwa kama kima cha chini cha wingi wa maji katika mto (minimum flow).

Hata hivyo, matokeo ya upimaji huo yalionesha kuwa Mbwinji yenyewe ilikuwa na uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 7,516.8 kwa siku, Rungwe mita za ujazo 777.6 kwa siku, Muungano wa Mbwinji na Rungwe mita za ujazo 8,380.8 kwa siku, Minjale mita za ujazo 3,196 kwa siku na muungano wa Mbwinji, Rungwe na Minjale mita za ujazo 13,651.2 kwa siku.

Kabla ya mafuriko ya mwaka 1990 chanzo cha maji cha mto Mbwinji kilikuwa kinatumika na mradi wa maji wa Makonde kupeleka maji katika vijiji 26 vya Wilaya ya Newala ambapo kiasi cha mita za ujazo 800 kwa siku zilitumika katika mradi huo.

Mahitaji ya maji kwa sasa kutoka kwenye mto huo yanaonesha kuwa mradi wa maji wa Makonde (vijiji 26) unazalisha mita za ujazo 800 kwa siku, mji wa Masasi mita za ujazo 6,000 kwa siku , mji wa Nachingwea mita za ujazo 5000 kwa siku, mazingira mita za ujazo 2,730 kwa siku (sawa na 20% ya kima cha chini ya maji ya mto).

Vile vile, vijiji 4 vya wilaya ya Masasi mita za ujazo 800 kwa siku vijiji hivyo ni Chikukwe, Liloya, Maparangwe na Chanikanguo-Maili sita vyote vikiwa na watu 8,893 pamoja na vijiji tisa vya Wilaya ya Nachingwea mita za ujazo 1,500 kwa siku ambavyo ni Chiumbati Shuleni, Chiumbati Miembeni, Songambele, muungano , Nangowe Shuleni, Nangowe Matangini, Stesheni na Chemchem vyote vikiwa na watu 17,700.

Kwa takwimu hizi, maji ya mto huu yanaweza kutosheleza mahitaji ya miji ya Masasi na Nachingwea kwa asilimia mia moja kwa miaka michache ijayo.

Hata hivyo, ikiwa mradi wa maji wa Makonde utachukua tena maji basi kiasi cha maji ya mazingira kitashuka hadi kufikia silimia 13.6 kutoka asilimia 20 inayokubalika. Endapo mahtaji ya maji ya vijijini yatajumuishwa katika ujenzi wa miradi ya maji ya Makonde na miji ya Masasi na Nachingwea basi maji ya mto yaliyopo hayatatosheleza.

Wakati wa ziara yake katika chanzo hicho cha maji cha mto Mbwinji Dk. Shukuru Kawambwa mbali na kukabiliwa na maombi ya kutoka kwa wananchi wa Wilaya hizo mbili za Masasi na Nachingwea kutaka kupatiwa mradi wa maji wa Mbwinji, aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Masasi pamoja na Ofisi ya Bonde la Mto Ruvuna na Pwani ya Kusini kuanza mikakati ya kukitambua chanzo hicho.

Dk. Kawambwa ambaye alikuwa waziri wa kwanza kukitembelea chanzo hicho tangu kituo cha kudumu cha kupimia maji katika chanzo cha maji cha mto Mbwinji kisombwe na mafuriko zaidi ya miaka kumi na saba iliyopita alisema, utambuzi wa chanzo cha maji cha Mbwinji utawezesha mamlaka husika kuhifadhi na kuepuka uvamizi wowote unaoweza kufanywa na wananchi hasa kipindi hiki ambacho Serikali inataka kukiendeleza.

Alimtaka mkuu wa Wilaya ya Masasi bw. Said Amanzi pamoja na Afisa bonde wa Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini bw. Aloyce Kapanda kufuatilia haraka utambuzi wa chanzo hicho ili hatua za haraka zianze kuchukuliwa mara moja.

Aliongeza kwa kusema utaalamu wa Mamlaka hizo utasaidia kuelewa eneo gani katika chanzo cha maji cha mto Mbwinji litambuliwe na lipi lisitambuliwe.

Pamoja na chanzo cha mto huo kuonesha kuwa na maji mengi lakini kinakabiliwa na matatizo kama shughuli za kilimo katika maeneo yanayozunguka chemchem ambazo zinaathiri ubora na uwingi wa maji, Ujenzi wa makazi katika eneo la chemchem unazidi kuharuibu mazingira na kupungua kwa maji, ukataji miti kwa ajili ya mbao na uchomaji moto misitu unaathiri sana mazingira na kusababisha kupungua maji pamoja na kuharibika kwa barabara ya kufikia kwenye chanzo kunazuia ukaguzi wa kwa mara wa chanzo.

Ingawa kuna dalili ya kuwepo mgogoro wa nani hasa anastahili kutumia maji ya chanzo cha maji ya mto Mbwinji baina ya wakazi wa Masasi na Nachingwea lakini Wananchi hao hawana budi kufahamu kuwa takwimu za kitaalamu zitakazotolewa na mamlaka husika juu ya matunmizi ya chanzo hicho ndiyo pekee yatakayotoa jibu ni maeneo gani yapate maji na si kila upande kutaka huduma ya maji ya chanzo hicho ielekezwe upande wake.