Sunday, 16 March 2008

Ukosefu wa maji huleta umasikini

Unapozungumzia umasikini basi ieleweke kuwa ni jambo linalozikabili nchini nyingi hususan zile nchi za dunia ya tatu Tanzania ikiwemo. Yapo mambo mengi yanayozungumzwa kuwa yanachangia kwa namna moja ama nyingine kushamiri kwa umasikini lakini kwa mtazamo wa wazi ukosefu wa maji unaweza kuwa moja ya sababu kubwa zinazochangia umasikini duniani.

Ieleweke kuwa Ulimwengu wote sasa unakabiliwa na upungufu wa maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu ikiwa ni pamoja na matumizi ya nyumbani, kilimo, usindikaji bidhaa viwandani na uzalishaji umeme. Kwa ujumla upungufu huo wa maji unaathiri maisha ya binadamu na mazingira.

Mbali na maji kuwa muhimu bado tunayapunguza kwa kuyamwaga ovyo, kuchafua vyanzo vyake, kukata misitu, kuchimba miamba hasa kwenye shughuli za uchimbaji madini pamoja na kutumia teknolojia za uzalishaji zinazotumia maji kidogo hasa viwandani na kwenye kilimo.

Maji ndiyo mhimili mkuu wa uchumi na yanapopungua husababisha umasikini wa kukithiri hivyo ni wajibu yatunzwe na kutumika kwa umakini.

Kwa kawaida mahitaji maji yanaongezeka wakati maji yenyewe yanapungua hali hiyo inasababisha migogoro katika jamii na migogoro hiyo inaweza kuwa kati ya watumiaji mbalimbali wa maji na nchi zinazomiliki vyanzo vya maji kwa pamoja hivyo jamii yoyote ikishakuwa na mgogoro haiwezi kufanya kazi yoyote ya uzalishaji na kuishia kuhangaikia umasikini.

Kwa kuwa maji ni muhimu, jamii nyingi zisizokuwa na huduma ya maji hutumia muda mrefu kutayatafuta badala ya kushughulikia masuala ya maendeleo, kwa maana nyingine mapungufu ya maji kwenye mito na mabonde hupunguza uzalishaji wa chakula hasa kwa wale wenye mashamba yanayozalisha kwa mwagiliaji.

Kwa zile sehemu zenye uhaba, maji huchotwa bila kubakizwa kwa ajili ya utunzaji mazingira hali inayosababisha wanyama na viumbe wengine kufa au kuhama.Kuna maeneo mengine vyanzo vya maji hutumika kupokea uchafu toka majumbani au kwenye mabwaya ya kusafishia maji taka.

Jamii ikikumbwa na janga la upungufu wa maji mara nyingi hutangatanga kama ilivyojitokeza nchini Tanzania mwaka 2006 ambapo wafugaji waliacha makazi yao na mali nyingine wakahama kutafuta maji. Jamii hii ilipoteza mifugo na kukosa huduma muhimu kama shule, hospitali na maduka ya kupata mahitaji.

Hali ya maji Tanzania inaonesha kuwa hadi kufikia Desemnba 2006 huduma ya upatikanaji maji mijini ilikuwa asilimia 78 na vijijini ni 55 wakati maji taka mijini ni asilimia 17 ingawa kiwango nkilichoainishwa ni kidogo lakini bado nchi ina vyanzo vya maji vya kutosha.

Hata hivyo, utafiti unaonesha kuwa tukigawana maji yanayoingia kwenye vyanzo vya maji kwa mwaka kila mtanzania atapata lita milioni 2.7 kwa mwaka ambayo ni sawa na lita 670 kwa siku inayojumuisha matumizi ya maji yote. Ingwa Tanzania kuna maji mengi lakini hayajasambaa kwa usawa katika sehemu zote nchini kwani Sehemu za kati kati ya nchi zinapata mvua kidogo ukilinganisha na maeneo mengine..

Katika mfumo wa usambazaji maji nchini kwa matumizi ya kawaida inakadiriwa kupoteza wastani wa asilimia 30-50 huku umwagiliaji nao ukichukua asilimia 70-85. Sehemu nyingine zinajumuisha uharibifu miundo mbinu, ukosefu wa kufanya matengenezo wa mfumo wa usambazaji pamoja na kutolipwa kwa gharama halisi ya kupata maji.

Hata hivyo, mbinu mbalimbali zinaweza kutumika ili kupunguza upotevu wa maji na baadhi yake ni kutumia maji kidogo, kupanga mipango ya matumizi ya ardhi inayozingatia uhifadhi wa vyanzo vya maji , kutumia maji kwa uangalifu, kupunguza yanayovuja, kuchagua teknolojia isiyotumia maji mengi , kuchagua kilimo kisichotumia maji mengi na kuwa na mifugo inayolingana na uwezo wa eneo.

Aidha, vyanzo vya maji mbadala pia ni muhimu katika kupambana na upungufu wa maji vyanzo hivyo ni pamoja kusafisha maji taka, kutumia maji ya bahari, kuchimba visima virefu hadi vya mita 1000 kwenda chini ya ardhi, kutumia wataalamu wa kumwagia mashamba wa matope(drip irrigation)

Vile vile, kuhusisha jamii katika kubuni, kujenga na kuendesha miradi ya maji hasa maeneo ya vijijini. Utaratibu huu utaimarisha uwezo wa wananchi kumiliki na hivyo kupunguza uchimbaji wa miundo mbinu .

Elimu kwa watu wa mijini itiliwe mkazo huku watu hao wakielimishwa umuhimu wa kulipa Ankara za maji wanayotumia, utunzaji ushirikishe sekta nyingine zinazohusika na matumizi ya vyanzo hivyo mfano sekta ya kilimo na ufugaji, misitu, madini na ardhi.

Kwa kuhitimisaha naweza kusema kuwa upatikanaji maji ya kutosha na salama kwa matumizi mbalimbali ni muhimu katika kuleta maendeleo ya kupunguza umasikini hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kupambana na tatizo la upungufu wa maji katika kuleta maendeleo, kuondoa umasikini , kupunguza maradhi sambamba na kuongeza uzalishaji mashambani na viwandani.

Matumizi sahihi ya maji ni kupunguza upotevu wa maji utakaowezesha taasisi zinazosimamia na kutoa huduma ya maji kupata fedha za kufanya matengenezo na kupanua miundombinu.

No comments: