Sunday, 16 March 2008

Ziara ya Dk. Kawambwa Misri iwe changamoto

Dk. Shukuru Kawambwa na Waziri wa Rasilimali za Maji na Umwagiliaji wa Misri Dk. Mahmoud Abu-Zeid wakisaini mkataba. Hapa ilikuwa jijini Cairo, Misri.


Hivi karibuni aliyekuwa Waziri wa Maji Dk. Shukuru Kawambwa alifanya ziara ya siku tano nchini Misri kwa mwaliko wa Waziri wa Rasilimali za Maji na Umwagiliaji wa Serikali ya Misri, Dkt Mahmoud Abu-Zeid.

Ziara hiyo ililenga kufuatilia utekelezaji wa maafikiano yaliyofikiwa baina ya Tanzania na Misri wakati wa ziara ya aliyekuwa waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo mwaka 2004, Mhe. Edward Lowassa, pamoja na kuangalia jinsi ya kuimarisha na kupanua ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Katika ziara hiyo Dk. Kawambwa na mwenyeji wake Dk. Abu-Zeid walipitia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa mwaka 2004, ambapo baadhi ya mambo yaliyokwishatekelezwa ni kupatiwa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalamu 16 wa kitanzania kuhusiana na maji shirikishi, mazingira, maji kwenye maeneo kame na kilimo cha umwagiliaji sambamba na mradi mpya wa kutathmini rasilimali za maji chini ya ardhi kwa Bonde la mto Nile kuanza kutekelezwa mwaka huu wa fedha 2007/2008.

Akiwa nchini Misri, Dk. Kawambwa na Dkt Abu-Zeid walisaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa uchimbaji visima 30 kwenye Wilaya kame nchini. Jumla ya Wilaya 6 zitanufaika na mradi huo. Wilaya hizo ni Same (Kilimanjaro), Kiteto(Manyara), Tarime na Bunda (Mara), Maswa (Shinyanga) na Magu (Mwanza).

Wakati wa utiaji saini mkataba huo, Mhe. Kawambwa aliwasilisha rasmi ombi kwa Serikali ya Misri kusaidia kuchimba visima vingine 70 kwenye maeneo kame nchini Tanzania ili kuwaondolea kero ya maji wananchi wa maeneo husika.

Uchimbaji huo visima siyo tu utawaondolea kero ya muda mrefu ya maji katika maeneo hayo bali utapunguza lawama za muda mrefu zinazoelekezwa kwa mamlaka husika pamoja na serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi kuwa imeshindwa kuwapatia majisafi na salama kama ilivyoainishwa katika ilani yake ya chama.

Mbali na kutiwa saini mkataba huo utakaoleta nafuu ya maji kwa wale wananchi wanaoishi maeneo kame tumaini lingine ni ile ahadi iliyotolewa na wataalamu washauri wa mradi wa maji Chalinze kuwa wanaandaa ratiba mpya itakayoonesha jinsi watakavyokamilisha kazi ya usanifu ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Ahadi hiyo inatokana na Dk. Kwambwa kutoa agizo kwa wataalamu washauri wa mradi huo wa Chalinze ambao ni Dk.Ahmed Abdel Warith Consulting Enginerrs, kampuni inayosanifu ujenzi wa mradi huo.

Wataalamu washauri hao bado walikuwa hawajawasilisha Wizarani taarifa muhimu za hatua ya kwanza, jambo lililoelezwa limekwamisha awamu ya pili ya mradi wa Chalinze kuanza katika muda uliopangwa suala lililomlazimu Dk. Kwambwa kuwataka washauri hao kuhakikisha usanifu unakamilika Novemba 30 mwaka huu ili kuruhusu zabuni za ujenzi kutabngazwa Desemba mwaka huu..

Pia Dk. Kawambwa na ujumbe wake walitembelea Kituo cha Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji, kituo kinachofuatilia hali ya hewa na rasilimali za maji nchini Misri ambapo madhumuni yake ni kupata takwimu muhimu kwa kutumia njia za kisasa kama Satelite kwa ajili ya kuzitumia katika usimamizi na udhibiti wa rasilimali za maji. Kituo hicho pia kinafuatilia miradi yote ya umwagiliaji ili kuwa na uwiano mzuri wa matumizi ya maji yanayopatikana.

Kituo hicho ni moja ya changamoto kwa Tanzania kuanza kufikiria namna ya kuwa na kituo cha aina hiyo ili kuweza kufuatilia hali ya hewa na rasilimali za maji kwa lengo la kufahamu na kuzitumia vyema rasilimali zilizopo hapa nchini kwa ajili ya kizazi kilichopo na kijacho.

Aidha, alitembelea pia Benki ya Taifa ya Takwimu za Rasilimali za Maji na Umwagiliaji, Benki hiyo ina taarifa zote kuhusu mitaro na njia zote za umwagiliaji wa maji kwenye mashamba, maji chini ya ardhi, uondoaji majitaka, majitaka kutoka viwandani, mazingira na hali ya uchumi.

Mbali na mambo mengine, Mhe. Kawambwa alipata nafasi ya kujionea kituo cha kutabiri masuala ya hali ya hewa na muelekeo kuhusu vyanzo vya maji ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana kutoka kwenye satellite, kituo hicho hutumika kutabiri muelekeo kuhusu mawingu na hatimaye makadirio ya kiasi cha mvua na maji kwenye kijibonde cha mto Nile. Takwimu hizo husaidia kukadiria kiasi cha maji yanayoingia kwenye bwawa la Aswani. Dk. Kawambwa na ujumbe wake walifarijika kuona umuhimu wa kuwepo kituo kama hicho nchini Tanzania kwa kuwa ni kiungo muhimu kwa ajili ya vyanzo vya maji.

Vile vile, Dk. Kawambwa na ujumbe wake walitembelea Kituo cha Kitaifa cha Tafiti za Maji chenye taasisi 12 chini ya udhamini wake. Baadhi ya Taasisi hizo ni Taasisi ya Tafiti za Rasilimali za Maji, Maabara Kuu ya Usimamizi wa Mazingira na Taasisi ya Tafiti kuhusu Miundombinu ya Maji iliyokubali kutoa msaada kwa Tanzania kufanya matengenezo ya vifaa vinavyotumika kupima wingi wa maji kwenye mito.

Alijionea pia mradi wa kuendeleza Sinai, mradi unaosimamiwa na Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji unaolenga kuanzisha maeneo mapya ya kilimo katika ekari 400,000 katika maeneo ya jangwa yaliyopo Sinai, lengo likiwa kupanua wigo wa Bonde la mto Nile na hivyo kuvutia wananchi kuhama kutoka Nile kwenda maeneo ya Sinai.

Ziara ya Waziri wa Maji ilihitimishwa kwa kutembelea shughuli za Kituo cha Kanda cha Mafunzo kwa Watumishi wa Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji nchini Misri, kituo kilichoanzishwa mnamo mwaka 1994 na kuchaguliwa na UNESCO 2002 kuwa Kituo cha Kanda kwa maeneo ya jangwa ya Afrika na nchi za Kiarabu na tayari kituo hicho kimekwisha kutoa mafunzo kwa wanafunzi kutoka Tanzani.

Yote haya aliyojionea Mhe. Kawambawa na ujumbe wake nchini Misri ni changamoto tosha kwa nchi yetu kuanza kuwa na mawazo ya kuwa na vitu vinavyoendana na teknolojia ya sasa katika kuafutialia na kuhifadhi rasilimali za maji ili kuepuka matatizo ya mara kwa mara ya ukosefu wa maji.

Hali hiyo inatokana na kuwa pamoja na Tanzania kuwa na matatizo ya maji lakini kuna taarifa kuwa Tanzania ni moja ya nchi katika Bara la Afrika yenye maji mengi chini ya ardhi ingawa bado hajagunduliwa.

No comments: