Sunday, 13 April 2008

Mafuriko Kyela

Pichani baadhi ya wananchi wakijaribu kuvuka mto. Kidaraja hicho sasa hakipitiki tena. Picha kwa hisani ya Mjengwa

Mvua za masika zimezidi kupamba moto nchini na zimekuwa zikisababisha mafuriko sehemu mbalimbali. Baadhi ya maeneo ambayo yamepata mafuriko ni pamoja na Vunjo, Same na Kyela. Hata hivyo hadi hivi sasa ni wilaya ya Kyela ambayo ina kata 15 ambazo kati ya hizo 11 zimepatwa na mafuriko makubwa .

Siku ya Jumamosi nimepata nafasi ya kuzungumza na Mbunge wa Jimbo la Kyela Dr. Harrison Mwakyembe (CCM) kuhusu athari za mafuriko hayo na mahitaji ya msaada. Kwa kifupi hali ilivyo ni kuwa:

a. Kaya 9000 hazina mahali pa kuishi, zimekosa chakula, au athari ya moja kwa moja iliyotokana na mafukio hayo

b. Hadi hivi sasa watu wawili wamefariki

c. Madhara makubwa katika mashamba ya mpunga kiasi kwamba kuna uwezekano kuwa kwa mara ya kwanza Kyela itahemea chakula mwaka huu.

d. Mvua kubwa namna hii hazijawahi kunyesha Kyela kwa karibu miaka thelathini sasa.

e. Juhudi za kuleta misaada zinaendelea ambapo JWTZ imepeleka kikosi chake cha Uhandisi, huku Msalaba Mwekundu wakiandaa misaada ya vitu mbalimbali.

Dr. Mwakyembe anaomba msaada wa Watanzania wote popote pale walipo kuweza kusaidia wananchi wenzao ambao ni kama wamepatwa na "Kimbunga cha Katrina" kwani wengi sasa wanaishi makanisani na kwenye mashule na afya zao ziko hatarini hasa kutokana na uwezekano mkubwa wa kuibuka mlipuko wa magonjwa yanayoambukizwa kwa maji kama typhoid, kuhara damu, salmonella, na pia ongezeko la Mbu wasababishao Malaria.

Kwa yeyote aliyeko Dar, unaweza kutuma mchango wako kupitia:
Kyela Development Fund MNB Bank House Acct No: 2013300198
Au Wasiliana na Dr. Mwakyembe kupitia simu Namba: 255 754 284130kwa maelekeo ya kuweza kutoa mchango wako kupitia yeye mwenyewe

Tafadhali sikiliza mahojiano yangu na Dr. Mwakyembe. KLH News imeahidi kutoa msaada wa Shilingi laki mbili kama sehemu ya jitihada za kuwasaidia wananchi wa Kyela.



Habari hii ni kwa mujibu wa Mwanakijiji anayepatikana katika mtandao wa
http://mwanakijiji.podomatic.com/

No comments: