Tuesday, 1 April 2008

Ridley na Uislam

Bi. Vyonne Ridley akipata maelezo kuhusiana na maktaba ya Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM) kutoka kwa mkurugenzi wa maktaba ya chuo hicho Bw. Masawe (Kulia) huku Makamu Mkuu wa MUM Prof. Hamza Njozi akiangalia.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM) Prof. Hamza Njozi akimuongoza Bi. Ridley katika majengo ya idara ya Mawasiliano ya Umma ambapo huko kuna studio za Radio na Televisheni, Chumba cha Habari na chumba cha uhariri.




Bi. Vyonne Ridley




Waislamu nchini Tanzania wametakiwa kuungana pamoja ili kukabiliana na vitendo vyote vya ukandamizaji vinavyofanywa dhidi yao.

Hayo yalielezwa hivi karibuni na mwandishi maarufu kutoka Uingereza Bi. Vyonne Ridley wakati akihutubia maelfu ya waumini wa dini ya kiislamu katika mhadhara uliondaliwa na chuo kikuu cha waislamu Morogoro (MUM) uliofanyika ukumbi wa Star Light jijini Dar es Salaam.

Alisema, hivi sasa kumekuwepo ukandamizaji, uonevu na udhalilishaji unaofanywa dhidi ya nchi za kiislamu kutoka baadhi ya nchi hususan zile za magharibi jambo alilolieleza kuwa linahatarisha usalama wa waumini wa dini hiyo.

Bi. Ridley aliongeza kuwa, njia pekee ya kuweza kukabiliana na hali hiyo ni waislamu duniani kuwa na umoja kwa lengo la kuhakikisha hakuna ukandamizaji ama uonevu unaofanywa dhidi yao.



Mwandishi huyo wa habari maarufu kutoka Uingereza ambaye amesilimu Ukristo na kuwa Muislamu alisema, pamoja na awali kuelewa waislamu ni magaidi na watu hatari lakini alipotekwa na wanamgambo wa Taliban aligundua ni watu wakarimu tofauti na inavyoenezwa.

‘’Nilichogundua nilipotekwa na wanamgambo wa Taliban ni kuwa waislamu ni watu wakarimu, wazuri na wenye hekima tofauti na inavyooenezwa na baadhi ya nchi za magharibu kuwa ni watu hatari na magaidi’’ alisema Bi. Ridley.

Akiongea kwa hisia kali Bibi Ridley alibainisha kuwa, pamoja na kuelezwa waislamu ni magaidi lakini hadi hii leo mwandishi huyo hajapata tafsiri halisi ya neno gaidi kutoka kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair mbali na kuihitaji tafsiri hiyo mara kwa mara kutoka kwake.

Amewataka waumini wa dini ya kiiislamu kumtii mwenyezi mungu na kuyafuata mafundisho yake kwani anaamini kunusurika kwake alipotekwa huko Afighanistan ni uwezo wa mwenyezi Mungu na si mtu mwingine.


Katika mhadhara huo ukumbi wa Star Light ulifurika idadi kubwa ya watu huku baadhi yao wakimua kuondoka kutokana na kukosa nafasi. Hata pale Bibi Ridley alipomaliza kutoa mhadhara watu walitaka aendelee jambo lililomlazimu Makamu mkuu wa chuo cha waislamu Morogoro Prof. Hamza Njozi kuingilia kati na kuwasihi kuwa muda wa sala ulikuwa umefika na katika mambo yanayoweza kuahirisha sala mhadhara haukupewa nafasi.

Baada ya kauli hiyo ya Prof Njozi, wanawake walimfuata Bibi Ridley na kumzonga kwa shauku ya kutaka kusalimiana naye jambo lililomuweka katika wakati mgumu mgeni huyo ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuitembelea Tanzania.

Baadhi ya waislamu waliozungumza na gazeti hili la Baraza wakati wa mhadhara huo waliomba Bi.Ridley kuendelea na ziara yake nchini na kuonana na makundi mbalimbali .

Bi. Ridley alikuja nchini kwa mwaliko wa Chuo kikuu cha waislamu Morogoro na kuanza ziara yake chuoni hapo na baadaye mbuga za wanyama Mikumi, Dar es Salaam na kuhitimisha huko Zanzibar.

No comments: