Sunday 16 March 2008

Maji yaja Shinyanga

Bwawa la maji la Zanzui Wilayani Maswa mkoa wa Shinyanga ambalo liko katika hatua za mwisho kukamilika.

Mwishoni mwa mwaka jana (2007) aliyekuwa Waziri wa maji Dk. Shukuru Kawambwa alifanya ziara katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Mara na Shinyanga, lengo la ziara hiyo ilikuwa kukagua ujenzi wa miradi ya maji pamoja na kuzindua visima.

Katika ziara hiyo Waziri wa Maji alitembelea Wilaya za Same (Kilimanjaro), Bunda na Serengeti (Mara) pamoja na Bariadi, Maswa , Meatu na Kishapu (Shinyanga).

Dk. Kawambwa katika ziara yake hiyo alikagua mabwawa ya Nyambele na Kinyambwiga yaliyoko wilayani Bunda, Mugumu (Serengeti), Zanzui (Maswa) na bwawa la Mwanyahima lililopo Meatu.

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la uharakishaji upatikanaji maji safi na salama kuwa wananchi wa wilaya husika katika muda muafaka kama ilivyoainishwa katika Sera ya Maji ya mwaka 2006-2025.

Miradi yote aliyoikagua Dk. Kawambwa pamoja na ule mradi mkubwa wa maji wa Kahama-Shinyanga inatarajiwa kukamilika mwaka huu 2008 na mara itakapokamilika tatizo la maji katika mkoa wa Shinyanga linaweza kubaki historia.


Mbali na juhudi za kuupatia mkoa wa Shinyanga maji, Dk. Kawambwa alisema serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 359 kwa ajili ya kuboresha huduma ya majisafi na salama nchini Tanzania.

Alisema kupitia kiasi hicho cha pesa kila wilaya imetengewa fedha kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji na kueleza kuwa tayari shilingi bilioni 19.5 zimegawanywa mwaka 2007 kwa zile halmashauri zilizokidhi vigezo vya kupatiwa fedha hizo.


Hata hivyo, Dk. Kawambwa alisema bado wananchi wana deni kubwa kwa wafadhili na wahisani juu ya miradi ya maji inayozinduliwa na kueleza kuwa kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanaunda vyombo vya kisheria vitakavyosimamia na kuendesha miradi ya maji.

Cha msingi kwa wananchi wa Tanzania mara baada ya kukamilika kwa miradi yote ya maji ni kutunzwa sambamba na kuanzishwa kamati za maji zitakazokuwa na jukumu la kusimamia na kuiendesha miradi hiyo ili iwe endelevu.

Pia wananchi hawana budi kushirikiana na serikali kwa kuacha kuendesha shughuli zozote kwenye vyanzo vya maji ikiwemo ufugaji na shughuli nyingine ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaweza kusababisha vyanzo hivyo kuharibika.


No comments: