Sunday 16 March 2008

Mbunge huyu awe mfano

Dk. Shukuru Kawambwa akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa Same Mashariki wakati akizindua miradi ya maji ya kisima iliyojengwa kwa juhudi za mbunge wa jimbo hilo Bi. Anne Kilango Malecela.



Mwishoni mwa mwaka 2007 aliyekuwa Waziri wa Maji Dk. Shukuru Kawambwa alifanya ziara katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Mara na Shinyanga, ziara iliyokuwa na lengo la kukagua ujenzi wa miradi ya maji pamoja na kuzindua visima vya maji.

Kati ya mikoa hiyo aliyotembelea mhe. Waziri wa Maji mkoa wa Kilimanjaro ziara yake ilielemea zaidi kwenye uzinduzi wa visima tofauti na mikoa mingine.

Wilayani Same katika jimbo la Same Mashariki Dk. Kawambwa alizindua jumla ya visima ishirini vyenye thamani ya shilingi milioni 40 kwenye tarafa ya Gonja katika zile kata za Mtii, Bombo, Vuje pamoja na ile tarafa ya Ndugu kata ya Kihurio.

Visima vyote alivyozindua Dk. Kawambwa vimefungwa kwa pampu za mkono na kufuata vyanzo vya asili lengo likiwa kurahisisha upatikanaji maji hasa ikizingatiwa upatiakanaji maji chini ya ardhi ya milima ni migumu.

Miradi hiyo ya visima iliyozinduliwa Wilayani Same imeinua asilimia ya upatikanaji wa maji ya bomba kutoka makisio ya asilimia 5 katika kata ya Mtii hadi 30, asilimia 20 kata ya Vuje hadi 35, asilimia 43 kata ya Kihurio hadi 62 na ile asilimia 12 kata ya Bombo hadi 25.

Kwa sasa asilimia 70 ya wananchi wa jimbo la Same Mashariki wanaishi milimani ambako kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa maji na kusababaisha asilimia 30 ya wakazi wa eneo hilo kupata magojwa yanayotokana na maji yasiyo salama.

Kwa ujumla wilayani Same kuna matatizo ya maji ambapo eneo la Tambararre ya Pare na milima ya kijiji cha Kizungo linakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.

Wakati wa ziara yake katika jimbo hilo la Same Mashariki Dk. Kawambwa alipongeza jitihada binafsi za mbunge wa jimbo la Same Mashariki Bi. Anne Kilango Malecela za kuasaidia upatikanaji huduma za majisafi na salama katika jimbo lake kutoka asilimia 46.5% hadi 49%

Pongezi hizo za Waziri wa Maji kwa mhe. Anne Kilango Malecela zinastahili kabisa kwa kuwa mbunge huyo alipagana kufa na kupona kuhakikisha anawapatia wapiga kura wake huduma ya majisafi pasipo kuitegemea zaidi serikali.

Nilipozungumza naye, mbunge huyo wa jimbo la Same Mashariki alisema anajisikia faraja sana anapoona wapiga kura wake wanapata huduma ya majisafi na salama jambo alilosema lilikuwa likimuumiza kichwa kwa muda mrefu.

Aliongeza kwa kusema, upatikanaji huduma hiyo ni jitihada yake binafsi ya kusaka wafadhili wa kumsaidia kuwapatia huduma hiyo ya maji wananchi wake ambayo imekuwa adimu jimboni mwake na wilaya nzima ya Same.

Aliyataja baadhi ya makampuni yaliyomsaidia kufadhili ujenzi wa miradi hiyo ya visima kuwa ni kampuni za simu za Tigo na Vidacom, mamlaka ya Bandari Tanzania (PTA) pamoja na kampuni ya kifaransa ya Express Lited.

‘’Makampuni ya ndani nayo yanafadhili sana ili mradi mtu ujue namna ya kuandika proposal yako’’ Alisema Bi. Kilango

Alieleza kuwa, mkakati wake wa kuawapatia wananchi wa jimbo la Same Mashariki huduma ya majisafi umelenga kwenda kata hadi kata na kuongeza kuwa yeye akiwa mbunge atajisikia faraja sana pale atakapoona wapiga kura wake wanapata huduma ya majisafi na salama katika kiwango cha asilimia mia moja.

Kwa upande wake Dk. Kawambwa alisema katika kuhakikisha tatizo la maji linatokomezwa mkoani Kilimanjaro serikali iko mbioni kuanzisha mradi mkubwa wa kitaifa unaojulikana kama mradi wa Tambararre ya Pare, mradi unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 38.

Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, mradi huo utakapokamilika utanufaisha vijiji 36 kutoka wilaya za Same na Mwanga zilizoko mkoani Kilimanjaro na ile sehemu ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Vijiji vitakavyonufaika na mradi huo mkubwa ni vile vya Hedaru, Mabilioni, Gevao, Makanya,Mgurasi,Bangalala,Chajo,Mwembe,Njoro,Ruvu mferejini,Ruvu jiungeni,Majengo,Bendera,Mkonga Ijinyu na Mgandu vyote kutoka wilaya ya Same.

Vingine ni Kifaru,Kiruru Ibwejewa,Kisangara, Lembeni , Kiverenge,Kiti cha Mungu,Mbambua, Kileo,Kivulini,Kituri,Mgagao,Handeni,Langata Bora,Langata Kangongo, Nyabinda na kijiji cha Kirya vyote kutoka Wilaya ya Mwanga.

Kwa upande wa Wilaya ya Korogwe maeneo yatakayofaidika ni vijiji vya Bwiko,Mkomazi, Nanyogie,Manga, Mtindilio na Mikocheni

Waziri huyo wa Maji alibainisha kuwa, katika kuhakikisha mradi huo unaanza haraka tayari serikali imeomba ufadhili wa mradi huo kutoka Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA) ili isaidia ujenzi wa mradi.

Mbali na jitihada zinazooneshwa na serikali kuwapatia wananchi wa Wilaya ya Same huduma ya majisafi na salama lakini bado juhudi binafsi zilizooneshwa na mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Bi. Anne Kilango Malecela ambaye hivi karibuni alijipatia umaarufu katika sakata la Richmond zinapaswa kuigwa na wabunge wengine wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mara kwa mara tunashuhudia malalamiko ya baadhi ya wabunge kuilaumu serikali kushindwa kupeleka huduma kwa wananchi ikiwemo huduma ya majisafi na salama, kwa kiasi fulani lawama hizo zinaweza kustahili lakini isiwe kigezo cha mbunge kuacha kufanya juhudi za kuwapelekea maendeleo wapiga kura wake kwa kisingizio cha serikali kufanya kazi hiyo.

Iwapo wabunge wataiga mfano wa Bi. Anne Kilango Malecela basi uwezekano mkubwa wa Tanzania kupiga hatua katika nyanja tofauti ni mkubwa sana kwani kila mtu atakuwa anajua wajibu wake kama mbunge na kamwe hawezi kuwa tegemezi wa serikali.

Mbunge huyo machachari alisema mtazamo wake mkubwa kwa sasa kama mbunge ni kutaka kuwaona wapiga kura wake wakiishi maisha mazuri na kuondokana na umasikini na magonjwa ambavyo vyote kwa pamoja vinaweza kuwafanya warudi nyuma kimaisha.

No comments: